Kenya News in Swahili and English

Kupambana na ufisadi katika jamii ya Wakenya na Lydia Maala.

Ufisadi ni ugonjwa ambao umevamia nchi yetu ya Kenya. Hapa chini ni insha kutoka kwa mwanafunzi wa shule ya upili ya Sirende kule Webuye. Mawazo kama haya lazima tuyatilie maanani tukitaka kuangamiza ufisadi nchi Kenya. 

Ufisadi ni aina mojapo ya balaa na beluwa inayokumba jamii yangu. Ufisadi ni kitendo ambacho hakistahili kutendwa katika Jamhuri hii yetu ya Kenya. Ni dhahiri kwamba wanafunzi wengi katika kitongoji changu hupitia katika misitu na nyika ili kuweka bidii ya mchwa masomoni. Wazazi wao kila mara wana mpini mkononi wakifanya kazi kucha kutwa angalau watoto wao waelimike. Ajabu ni kwamba, wanagenzi hao baada ya kupasi mitihani hukaa nyumbani bila kazi. 

Kuna aina nyingi za ufisadi katika Jamhuri ya Kenya. Hizi ni kama kuzunguka mbuyu, kukubali kuzungukwa mbuyu, kuzembea majukumu, ubaguzi wa rangi, ukabila, ushirikishaji wa mapenzi, kufuja mali ya uma na kadhalika. Haya yote ni aina ya ufisadi unaowatumbukiza wananchi katika shida za nui. Ufisadi wa kupokea rushwa unasabishwa na wananchi walionafasika humu Jamhurini. 

Watoto wafanyapo mitihani na kufeli, wazazi wao hutoa rushwa kwa wenye vyeo ili watoto hao mbumbumbu waweze kupata nafasi za kazi. Kwa upande mwingine, mtoto aliyejitahidi na kusoma hajabahatika kwa chochote maishani. Wazazi huuza mali yote kwa sababu ya karo ya shule huku wakiwa na matumaini kwamba watoto wao watapata kazi na kuwaokoa maishani mwao siku za uzeeni.  

Hali hii huwafanya watoto waliojitahidi masomoni kuwa watu fukara. Waliobakia nyuma hujikuta wameacha shule kwa ukosefu wa karo na kwenda kuchunga ng’ombe au kuwa watumwa wa watu. Jambo hili limenitia wasiwasi sana kama mhusika. 

Ufisadi huu waweza kufutiliwa mbali kama viongozi walio na nyadhifa kazini kuelimishwa kwamba si vizuri kupokea rushwa au kutoa rushwa. Waelimishwe kwamba, ufisadi wa kutoa na kupokea rushwa unaumiza wananchi na itakuwa vyema kama hawatakubali ushirikisho. Licha ya kuelimishwa, kama wanafunzwa na hawazingatii na kuyatilia maanani, wanaohusika wapewe adhabu kali kama kufungwa ili iwe mfano kwa wengine. 

Wananchi waelimishwe kupitia redioni na vyombo vingine vya kutangaza. Watu kote nchini wajue si vizuri kutumia rushwa ndipo mtu apate kazi. Aina nyingine ya ufisadi ni ukabila. Ukabila ni ufisadi unaoleta taabu nyingi nchini. Ninasema hivi nikiwa na hamaki kubwa kama mwananchi wa Kenya. Utakuta mtu baada ya kujaribu kwa mapana na marefu jinsi ya kufaulu maishani wanaingiza ukabila katika shughuli zake.  

Wenye madaraka hutumia ukabila kuwakosesha wengine nafasi maishani. Misaada kutoka nchi zingine ikiletwa nchini hapa, inatakikana kupewa kwa wananchi wote kwa jumla. Badala ya kufanya hivyo, mtu anashughulikia kabila lake bila kujali makabilamengine. Misaada itagawanywa kwa wenye vyeo na makabila yao. Hao huendelea kupata vitu vya bwerere huku wengine wakila mwata.  

Fukara yeyote akijaribu kujitetea, ndio hao wanawatia kirago “nendeni tutawaletea” lakini hao huendelea kushughulikia makabila yao. Masikini hubaki wakiwa hawana chajio chochote. Ndipo kweli wahenga hawakudosari walipoamba “kitanda usichokilalia huwajui kunguni wake”. Baada ya maskini kungoja na kushindwa, hujaribu juu chini kujitafutia kwani ngoja ngoja huumiza matumbo. 

Mtu apewapo wadhifa fulani katika kitu, hushughulika na yanayompasa peke yake, kweli asiyekuwepo na lake halipo. Hana haja na wengine. Jamii yake kila mara unapoingia nyumbani mwao, huwakuta wamo furahani riboribo na waonapo maskini, wao hushikwa na vicheko vya Kwe! Kwe! Kwe! na masikini yu machozini mwa Kwi! Kwi! Kwi! 

Ufisadi huu wa ukabila utatupiliwa mbali kama wahusika watafunzwa jinsi ya kuishi katika umoja. Viongozi wasiotii sheria wafutwe kazi kwa minajili hawajui wanachofanya. Kama watafutwa kazi, litakuwa funzo kwa wengine wanaovunja sheria. Umoja unaweza kuletwa kwa njia nyingine kama kushirikiana katika michezo, nyimbo katika shule. Wanafunzi wataishi kwa umoja bila kujali kabila. Watakapokua na kuwa wakubwa, wataendeleza taifa bila ya ubaguzi wowote. Sasa watu wote waweza kuitikia mwito na kuukomesha ukabila barabara. 

Ufisadi mwingine ni wa ubaguzi wa rangi. Vita vitokeapo katika makabila, mtu anaposikia hayo, anajifanya kwamba mambo hayo ya vita hayamhusu ndwele wala sikio. Huyatia masikio yao nta na kushughulika na pilkapilka zake mwenyewe. Mtu akipewa cheo kama kile cha Urais hawezi kuleta amani katika nchi, badala yake anawapelekea rangi yake zana za vita kama vile bunduki, mishale na kuwapa maarifa ya kuweza kumshinda mwingine katika vita. 

Hata hivyo, wanadamu wengi hupoteza maisha yao kila siku kwa minajili ya ubaguzi wa rangi. Wananchi wangekuwa na furaha mpwitompwito kuona mtu kama Rais akitekeleza na kuendesha kazi yake sawasawa. Wananchi wote katika Jamhuri hii yetu ya Kenya ni sawa. Ubaguzi wowote hauhitajiki. Ukifanya hivyo, hata vita vikitokea kati ya nchi hii na nchi jirani, hautakuwa na shida yoyote ila watu wataungana pamoja na kupigana nao na kuwashinda kwani umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.  

Tutaendelea kuishi kwa amani na umoja na hata vizazi vijavyo pia vitafuata nyayo na kuishi kwa amani. Ushirikishaji mapenzi ni aina nyingine ya ufisadi. Mwanamke yeyote au kidosho anapojaribu kuomba kazi, viongozi wanaohusika wanafanya juu chini kuona kwamba huyu amekubali kuwa nao. Asipokubali atanyimwa kazi na jambo kama hilo si halali kulitenda. Mtu anapopewa cheo ndipo raha zake anaziponda. 

Wananchi wote pamoja na wakuu wote tuweze kukaa chini na kujadiliana jinsi tunavyoweza kuepukana na ufisadi. Wanafunzi wanapomaliza masomo yao, serikali iliyo mamlakani iwashughulikie katika kuwapa kazi. Wote tujaribu kwa udi na uvumba bila kubaidika kama ardhi na mbingu na kusahau yanayotupasa kutekelezwa. Vijana na wazee kwa jumla tuache uzembe na kulisukukma mbele gurudumu la maendeleo katika Jamhuri yetu.  

Vizazi vijavyo havitakuwa na shida kama ufisadi wa kimapenzi utaondolewa. Ninaendelea kuligusia jambo hili kwa vile ni la kutisha na kuogofya. Sisi sote tuungane kwamba mtu yeyote anapomaliza masomo hadi chuo kikuu aweze kupata kazi na kuendeleza mahitaji yake. Tukifanya hivi, hata jamii yangu itakuwa na moyo na waendapo shuleni watasoma kwa bidii na nchi haitakumbwa na tatizo lolote.Tukitaka ufisadi huu uondolewe, itatupasa kulitia fikirani jambo kama hili. 

Anapopatikana kiongozi yeyote anayelazimisha wasichana kushirikiana naye kimapenzi, afutwe kazi mara moja na iwe funzo kwa wengine. Wasichana nao wanapoulizwa kufanya mapenzi wakatae katakata na kuwashtaki kwa wenye nyadhifa za juu zaidi. Ufisadi mwingine ni wa kufuja mali ya umma. Wafanyikazi wengi kawaida hao hawafuati sheria zinazotolewa. Kiongozi anawaza kupewa pesa za mishahara ya wafanyikazi. 

Badala ya kuwapa pesa zote, huwapatia thuluthi ya pesa hizo na zingine huzitumia kwa mahitaji yake mwenyewe. Hiyo ni njia moja ya wizi wa mali ya umma. Wizi mwingine ni wa daktari kupewa madawa ili ahudumie wagonjwa mbalimbali lakini badala yake, huchukua na kuyapeleka katika duka lake la dawa ili yauzwe. Wakifanya hivyo wanaumiza serikali kwa sababu watakuwa wanapata mshahara mara mbili. Wizi wa tatu ni wa wizara mbalimbali kupewa magari haya yakutumia kama vile wizara ya elimu.  

Magari hayo yanapaswa kutumiwa kutembelea shule za msingi, za upili na vyeo mbalimbali. Wasitumie magari hayo kubeba wasafiri kwa malipo. Huu ufisadi utaweza kuondolewa kama wataweza kuchagua viongozi wanaojua ni waaminifu. Wachunguze mtu ndipo apewe kazi kama ya kuwa mkuu wa wizara fulani. Daktari yeyote ambaye ni mtumishi wa umma azuiliwe kuwa na duka lake la dawa. 

Daktari akiwa na duka lake, atachukua madawa ya serikali na kuweka kwenye duka lake. Daktari wa umma yeyote akipatikana na duka lake la dawa ashikwe na kupelekwa kotini. Polisi pia wawe makini kuchunguza ili kuhakikisha hakuna gari la serikali linalobeba wasafiri. Wasafiri nao wasome majina yaliyoandikwa kwenye magari ili kusiwe na shida yoyote. Msafiri anapoona kuwa ni la serikali, haifai kulisimamisha ili abebwe.  

Ufisadi wa mwisho ni wa kuzembea majukumu. Mtu anaandikwa kazi na serikali lakini hawezi kutimiza jinsi inavyotakikana. Mtu anakosa kwenda kazi bila sababu maalum. Anapoulizwa anasema alikuwa mgonjwa, kumbe alifanya kazi zake nyumbani. Kama ni kwenda kazini, hawezi kufika kazini kwa wakati unaofaa na tena huondoka kabla saa ya kazi kuisha. Ukijaribu kumuuliza sababu za kuondoka kwake mapema au kufika huku amechelewa atakujibu alikuwa na mgonjwa nyumbani aliyetakikana kuhudumiwa.  

Mtu hutumia mda wa kazi ya serikali kufanya kazi yake binafsi. Kuna watu huku wanamngoja awahudumie lakini yeye naye huku anajishughulisha na yake bila kujali wengine. Mfanyikazi wa aina hiyo anapaswa kunyimwa mshahara unaolingana na siku ambazo hakufanya kazi. Wakinyimwa mshahara watapata funzo na kuweka juhudi katika kazi ya serikali. Wakifanya hivyo na bado wanaendelea, ni sharti wafutwe kazi kwa minajili hawatosheki na ile wanayopewa.  

Wakubwa nao watalazimishwa kuwa karibu na wafanyikazi ili kuchunguza wakati wao waking’oa nanga katika kazi yao. Watu wote wakifuata na kutekeleza mambo hayo, wananchi wataishi maisha ya salama salimini. Watu wote katika Jamhuri yetu ya Kenya tukifuata yaliyosemwa mwanzoni, hakutakuwa na shida wala taabu hapa nchini. Tuweze kuyaweka katika vichwa vyetu na kufikiriwa daima dawama. 

Munala Wa Munala. 

Advertisements

AprilUTCbThu, 05 Apr 2007 22:12:19 +0000000000pmThu, 05 Apr 2007 22:12:19 +000007 19, 2007 - Posted by | Uncategorized

No comments yet.

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: