Kenya News in Swahili and English

Serikali Ya Wezi Na Wafisadi Nchini Kenya.

Kunao wanaosema kwamba, Mungu anapotaka kumharibu mtu, kwanza humfanya kuwa mwehu. Wako aliharibiwa akili na pesa ambazo aliyekuwa mtawala wa Kenya wakati huo Daniel arap Moi alimpatia. Wako alipewa wadhifa wa Mkuu wa Sheria. Hapo, Wako alionyeshwa mshahara mzito na marupurupu mengine ambayo huenda na vyeo nchini humu (Kumbuka majaribu ya Yesu jangwani). Domo la Wako lilijazwa chakula na akawa hana nafasi ya kuongea ila kwa kuitetea serikali.

Mwanasheria wa kutetea haki za kibinadamu alikuwa mamlakani bila kulalamika katu, wakati ukandamizaji mkubwa wa kisiasa ulikuwa ukiendelea. Huyu ni mtu ambaye alikaa kitako katika ofisi isiyokuwa mbali na jumba ambamo kulikuwa na vizimba vya kuwatesa wapinzani wa serikali. Huyu ndiye mtetezi wa utu na haki ambaye alinyamaa huku haki ya kujieleza ikiwa ni haramu. Huyu ndiye mwenye haki ambaye hata hakushutumu mazoea ya kuwapeleka watu mahakamani usiku.

Huyu ndiye wakili ambaye alibadilisha neno fulani katika kifungu cha sheria ili kutoa faida kwa chama tawala KANU mara tu kabla ya kura za mwaka wa 1992. Yeye ndiye aliyekuwa akitoa uhalali kwa kazi ya watu ambao sasa ni mawaziri katika serikali hii, ambao walikuwa wahudumu katika kitengo cha utesaji wa wapinzani wa serikali kule katika jumba tukufu la Nyayo! Kumbuka kuwa Wako ndiye aliyeishauri serikali kuwa malipo yaliyotolewa kwa kampuni ya Goldenberg International yalikuwa halali.  

Serikali hii ambayo inaendesha shughuli za taifa sasa, na ambayo tumeambiwa mara nyingi kuwa ni mpya ilipochukua madaraka, ya kututawala, ilikuwa ni ajabu kuona kuwa huyu mpiga tabasamu alikuwa bado ndiye mkuu wa sheria. Kumbe dalili ya mvua ni mawingu. Sikujua kwamba serikali hii ilikuwa inamtafuta mtu ambaye ataweka mhuri wa uhalali kwenye shughuli ambazo ni haramu! 

Basi zilikuja kasheshe za Anglo Leasing na zinginezo ambako pesa ninazokatwa kila siku na serikali hii yenye uchu mwingi wa pesa, zinaishia tu mifukoni mwa matajiri walafi ambao nimelazimishwa kuwaita waheshimiwa. Katu siwaheshimu, kuanzia mkubwa wao, kupitia huyu mwingine mwanatabasamu, hadi chini kwa vibaraka wao wanaowatungia mashairi na kuwaongoa kwa maneno mazito wasiyokuwa na dhati ya roho nayo.

Injili Ya John Githongo: Katika taarifa tuliyopewa na aliyekuwa katibu wa kudumu wa maadili na utawala Bw. John Githongo, ufisadi ni jambo ambalo limelindwa kutoka ikulu, kupitia ofisi ya mpiga tabasamu, hadi kwenye vyombo vya dola. Ufisadi wa serikali ya NARC umepigiwa ua wa ukiritimba ambako kama wewe ni yahe, basi hufai kuwa fisadi. Mwachie mbunge wako, balozi, waziri au wanaotoka katika nyumba kubwa. Ukijaribu wewe utaumia. Tunaambiwa na Githongo jinsi rais mwenyewe anavyowajua marafiki zake wafisadi na kamwe hawezi kuwafuta.

Tunaambiwa pia kwamba mara tu baada ya kutawazwa, rais wangu alisahau kuwa nilimchagua kutokana na ahadi nzuri alizonipa, ahadi ambazo ziliambatana na ndoto za taifa hili nilipendalo kwa roho yangu yote. Badala yake, aliona kuwa alikuwa ameingia kwenye ghala la vinono. Alianza kupanga njama, yeye na watu wake, za jinsi ya kurudi ikulu kwa hongo. Licha ya kuwa yeye na watawala wenzake ni matajiri wakubwa, walilenga pesa ambazo zinafaa kununua madawa kwa masikini wanaoenda kwenye hospitali za umma, madawati, vitabu na vifaa vya kufundisha kwa shule za umma, kujenga barabara, kuanzisha miradi ya unyunyiziaji maji katika sehemu kame, kupambana na malaria, …… 

Je, utaamini kwamba Aaron Ringera ambaye ndiye mlinzi mkuu wa wafisadi atatoa faili inayotoa maongozi kamili dhidi ya wafisadi ambao anafanya bidii kuwaficha na kuwahifadhi? Si ajabu basi kuwa amempa mwenzake wa kutabasamu faili ambazo uchunguzi wake ni wa kutiliwa shaka. Ninaamini kuwa kwa kufanya mambo kama haya, Wako na mwenzake Ringera wangelipenda kuwachezea Wakenya mchezo wa mwajificho, ambako wanataka kupoteza muda ili tusahau kuwa tulikuwa tumewalenga wao.

Hebu fikiria, Ringera ni mtu ambaye amefuzu vizuri sana katika somo la sheria. Kabla ya kuingia katika shoroba za ufisadi, Ringera alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu katika idara ya sheria. Je, huyu ni mtu ambaye hajui mchakato wa kutayarisha faili za mashitaka? Kwa ujuzi alio nao, Ringera ni mtu ambaye anafaa kuwa hakimu. Ikiwa ametayarisha faili ambazo si kamili, basi kuna jambo ambalo ni la mchezo wa ping pong ili kuwahadaa wananchi wa kawaida.

Wino uliotumiwa kuandika orodha ya aibu ambayo ilisomwa hadharani na waziri wa haki na masuala ya katiba ulikuwa haujakauka wakati alipojipinda nyuma, na kuanza kusema kwamba miongoni mwa wale waliokuwa wametajwa (wale walioko serikalini) walikuwa hawana hatia.

Yeye Kama nani? Kwa misingi gani? Mbona wasifikishwe mahakamani ili vyombo vya dola vinavyotoa huduma za haki vipate kufanya kazi yao? Kwa kinywa chicho hicho, waziri na wenzake walikuwa wakipaaza sauti dhidi ya viongozi wa chama pinzani cha ODM-Kenya kuwa chama chao kilikuwa motoni kufuatia kuwa kwao kwenye orodha ya aibu.

Hebu fikiria, hata makamu wa rais Moody Awori naye alipayuka akisema kwamba wale viongozi wa ODM-Kenya waliotajwa kwenye orodha hiyo walikuwa wakikimbilia makabila yao kwa hifadhi. Je, wakumbuka yale makala ya kumtetea mwizi wa kabila langu? Je, wakumbuka ile kauli ya kusahau mabolozi wafisadi kama vile a liyekuwa balozi wa Kenya kule Scandinavia? Aliiba shamba la wakenya nab ado sasa hivi yeye ni huru kama kawaida. Kinyanjui, chako kii motoni!

Usiwe nyani wa kulichekelea kundu la mwenzio. Lako pia lachukiza ajabu.  Viongozi wa ODM-Kenya nao wakajipaka tope kwa kuwatetea wezi miongoni mwao wakisema kuwa kwa kuwa wao ni wafuasi na viongozi wa ODM-Kenya, basi hawangelikuwa na hatia. Katika somo la mantiki, hii ni mojawapo ya fikira lemavu na inapatikana kwenye kamusi ya fikira kama hizi. Je, unakumbuka hatima ya matokeo ya uchunguzi wa kashfa ya Anglo Leasing? Je, unajua kuwa aliyekuwa waziri wa fedha wakati wa Goldenberg George Saitoti hawezi kushitakiwa tena? Basi niambie ulitarajia nini kutoka kwa Amos Wako?

Unakumbuka usuhuba kati ya waziri Soita Shitanda na Wako? Mojawpo ya watu ambao walikuwa wametajwa katika orodha ya Maina Kiai (mwenyekiti wa tume ya kutetea haki za kibinadamu) ni Soita Shitanda. Soita alipoliona jina lake kwenye orodha hiyo, alitisha kujiuzulu ikiwa angelifikishwa mahakamani kwa kosa la udanganyifu ambao ulifanya serikali kumlipa pesa asizostahili. Wako alisema kwamba atachanganya sheria na huruma. Basi Shitanda aliambiwa kuwa alikuwa ametenda jambo lisilostahili kushitakiwa.

Je, hujaamini kuwa ufisadi ni biashara kiritimba ya viongozi wa serikali?  Tayari, Waluhya wameanza kusema kuwa Wako anaingiliwa kwa sababu watu fulani hawataki Mluhya kuwa Mkuu wa Sheria. Tayari nimeanza kupokea ujumbe mfupi kwenye simu yangu, unaonihimiza kumfuata Musalia Mudavadi kwenye jela ya Kamiti, ikiwa atahukumiwa kifungo kwa dhambi alizonitendea alipokuwa waziri wa fedha. Kwani mimi ninajichukia kiasi gani mpaka nimshangilie mwanakabila langu anaponinyonya bila aibu? Chambilecho wahenga, kama kimeoza tuba. Hapa Sweden, ubalozi wa Kenya unavunda  kama panya iliyokufa. Wakenya amkeni tujenge nchi yetu.

Munala wa Munala. 

Advertisements

AprilUTCbTue, 03 Apr 2007 23:01:04 +0000000000pmTue, 03 Apr 2007 23:01:04 +000007 19, 2007 - Posted by | Uncategorized

No comments yet.

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: