Kenya News in Swahili and English

TUWANG’ATUE WAZEE UONGOZINI NCHINI KENYA

Ni jukumu letu vijana wa Kenya kukataa katakata wanasiasa wote ambao wametimia miaka 65. Mifano ni kama Rais Mwai Kibaki, Moody Awori, Simon Nyachae, Ole Ntimama, John Michuki, Njenga Karume, Julia Ojiambo, Fred Gumo, Odhiambo Omamba, Musikari Kombo, Rahid Shakombo, Oburu Oginga, G. G. Kariuki, Mwendwa Nyiva, Chirau Mwakwere, Joseph Munyao, Oloo Aringo, Daudi Mwiraria, George Saitoti, Arthur Magugu, Noah Wekasa na wengineo. 

Tuyafumbue macho yetu na kutazama mbele. Hawa ni wachache miongoni mwa wazee wengi ambao waliingia uongozini tangu mwaka wa 1963, na hawana la kuonyesha Wakenya kimaendeleo. Lengo lao ni kujitajirisha na kuwalaghai Wakenya. Miongoni mwao, kuna wale ambao wameipora nchi yetu kwa miaka mingi. Je, mbona tuwarudishe wakorofi hawa uongozini tena? Amkeni vijana na muamue. 

Inastajaabisha kuona Wazee nchini Kenya wakimenyana na uongozi bila kuwaachia vijana nafasi ya kusaidia kwa ujenzi wa nchi yetu. Mzee mwenye busara akitimia miaka 65 ni lazima akae chini na watoto wake na awape wasia ili kuendeleza jamii. Kabla Mzee hajafa, ni wajibu wake kuwatolea wanawe maneno ya mwisho ambayo ni ya busara sana. Wazee kama hawa hawapo katika jamii ya siasa nchini Kenya. 

Vijana tunadhulumiwa

Asili ya maisha ya vijana wa Kenya ni ya shida, yenye kuchosha na mafupi. Vijana wanateswa sana na hata hawapewi nafasi ya kujieleza. Maoni yao yanatupiliwa mbali, sauti zao ni za wanyonge. Vijana wengi wanaishi katika hali ya utumwa na hawana uhuru. Je, hii ni sheria ya vijana? Je, ni kwa kuwa sisi vijana hatuna haki kama Wazee wetu? Nchi yetu ya Kenya imefanikiwa na utajiri mwingi sana. 

Vijana wa Kenya wanaweza kuishi maisha ya heshima. Yatupasa tusimame kama wabunge ili tung’ang’ane na hawa wazee ambao wameiharibu nchi yetu ya Kenya. Tukiungana pamoja tutawashinda kwa mlio mmoja. Shida nyingi zinazotukumba zinatokana na uongozi mbaya wa ukabila na ufisadi. Madawa ya kulevya ndio mengi kwa vijana, na sio ajabu kuona kwamba madawa haya husafirishwa na walio na fedha na vyeo vikuu serikalini. Lengo la viongozi hawa ni nini? 

Lengo lao ni kuwaangamiza na kuwachanganya vijana ili wasifahamu wanaponyimwa haki zao. Hao hawajali maslahi ya vijana, bora tu watimize malengo yao. Vijana tumeelimika na tuna ujuzi wa kuongoza Kenya. Tunaweza tu kama tutasambaza habari hii kwa sauti moja. Mapinduzi ya siasa nchini Kenya ndio majibu. Tupambane kufa na kupona ili tuokoe nchi yetu. Baada ya mapambano, tutasherekea kuona kwamba, kila Mkenya ameongezewa posho yake mezani.

Vijana tugutuke

Tumedanganywa na kuporwa haki zetu, kwani tunatumiwa kama ngao wakati wa kura, kisha tunatupwa kama tambara mbovu. Haya ni maisha gani jameni? Amkeni vijana na tuimbe wimbo mmoja wa kuingia kwenye ikulu mwaka wa 2008. Tutashinda tukiweka tofauti zetu kando. Sisi ni wengi kuwashinda na hebu tutumie akili zetu ili tuwang´atue hao wazee. 

Kenya inahitaji mapinduzi ya kisiasa na wanasiasa wote ambao wametutawala kwa zaidi ya miaka ishirini watolewe na kupatiana nafasi kwa viongozi wapya, ili tuone kama tutakuwa na mabadiliko. Safari ya mapinduzi ni ndefu sana, na inahitaji watu ambao wanapenda nchi yetu. Ni wazi kwamba Wabunge wetu wa sasa hawapendi nchi yetu. Wengi wao wamewasafirisha watoto wao ili wasomee nchi za ng’ambo. 

Wakenya watapiga kura mwishoni mwa mwaka huu. Matumaini ya vijana ni kuona serikali ambayo itasambaza huduma karibu na wananchi. Mbali na hayo, vijana wana imani kwamba, serikali mpya italeta maendelo ya haraka kote nchini ili kujenga taifa letu. Vijana hawana cha kujivunia kwa hii Serikali ya Kibaki, kwani bado wanateseka kama kawaida, na maisha yao hayajabadilika hata kidogo. Kinyume na yale serikali inadai kuwa kuna ongezeko la posho kwa Wakenya, ukweli ni kwamba, watoto wa Kibaki na familia za matajiri ndio wanahisi hilo ongezeko. 

Wazee waondolewe

Tabia za wanasiasa wa Kenya ni za aibu na hazina ukweli wala uaminifu. Kama kuna aibu ambayo nchi yetu inao, basi ni hao wanasiasa tulionao sasa hivi. Wakenya wengi wanapenda kusikiza upuzi wa viongozi/wanasiasa kama vile Murungaru, Kiraitu, Biwott, Saitoti, Bro. Paul (Kamlesh Pattni) na wengineo, ambao tunawafahamu vyema kabisa. Hebu tujiulize, inawezekanaje kuwarudisha watu kama hao uongozini? Ni kwa sabubu sheria zetu zina kasoro au sisi wenyewe tuna kasoro? 

Huu ni uamsho kuwa, lazima tutizame swala hili kwa makini. Vijana tuamke kumekucha na tuwakatae hao washukiwa tuliwataja hapo awali ili Kenya isonge mbele. Ahadi wanazotoa ni za uongo na wanaendelea ‘kutu-enjoyi’ wakisema eti sisi ni viongozi wa kesho. La hasha! Viongozi wa kesho wanaanza leo. Tuwang’oe hao wazee uongozini. Wametupotosha kwa miaka mingi sana na leo ni wakati wetu. Wazee kwaherini na ahsanteni sana kwa kazi mbaya ambayo mmefanya. 

Munala Wa Munala (kajamii@yahoo.com

Advertisements

MarchUTCbWed, 07 Mar 2007 22:14:14 +0000000000pmWed, 07 Mar 2007 22:14:14 +000007 19, 2007 - Posted by | Elimisha, Uncategorized

No comments yet.

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: