Mwaka wa Mavuno Kwa Wakenya
Mweka hazina wa chama cha Orange Democratic Movement-Kenya Scandinavia (ODM-KS) Bi. Sofia Njoroge, amesema leo kuwa ni jambo la busara sana Wakenya kuungana pamoja na kusaidiana ili kujenga nchi yetu ya Kenya. Bi. Njoroge amesema haya wakati ambapo chama chake cha ODM-KS kimeweka mpango kamili wa kutoa masomo ya bure kwa Wakenya hapa Sweden.
Aliendelea kusema kwamba Wakenya wajitoe kwa wingi na kujiunga na mradi huu wa masomo, kwani ni muhimu sana kuelimika. Serikali ya sasa imeshindwa kuwapatia Wakenye haki zao na ODM-K ikichukuwa uongozi, tutaona mabadiliko makuu. Tusiendelee kukaa hapa na ndugu zetu wanaangaika.
Ni aibu kubwa sana kuona viongozi wa Kenya wanaiba pesa na kuzikuficha nchi za ugenini na kuwanyima Wakenya mali yao. Viongozi kama Saitoti, Murungaru, Biwott na hata Moi, wanatia nchi yetu aibu kubwa sana. Hawa ni watu ambao wameiba nchi yetu na kule walikoficha hizo pesa, wemefungiwa kuingia ili kuzitoa, alisema Bi. Njoroge.
Mtu kama Moi akiumwa anakimbilia Ujerumani baada ya kunyimwa kibali cha kwende uingereza. Mbona wezi kama yeye wasijenge hospitali nzuri kama zile wanazokimbilia ng’ambo? Wakenya tujitoe na tusimame wima kwa kupigania haki zetu. Ni aibu sana kwenda kwenye hospitali kuu ya serikali na kuambiwa hakuna dawa, lakini unaweza kuipata kwa hospitali za kibinafsi. Mbona tunafanya biashara na maisha ya watu maskini? Hali hii itaendelea hadi lini?
Wakenya tusibabaishwe bure, turudi nyumbuni na kuchukua uongozi wa nchi yetu. Turudi nyumbani na tuchukue vyeo vya kisiasa na tuwafunze jinsi ya kuwaongoza Wakenya. Hivi majuzi tuliona vile serikali ya Kibaki ililazimisha wachumi kutengeneza numerali za ajabu za kuonyesha kuwa uchumi u sawa. Ukweli ni kwamba Wakenya wa kawaida bado hawana mafuta, chakula, madawa na hata karo ya kulipa shule.
“Kundi la NARC-KENYA ni lingine ambalo limeonja matamu ya siasa, ndoto yao ni kwamba Kenya ni ya Wakikuyu na familia zao. Tukatae hili kundi kwa sabubu ni kundi la kuwatenganisha Wakenya ambao wanapendana”, alisema Bi. Njoroge.
Munala Wa Munala (kajamii@yahoo.com)
“Tutaangamiza Ujinga Skandinavia,” Asema Bi. Hellen Opwapo
Mwenyekiti wa chama cha Orange Democratic Movement-Kenya Scandinavia (ODM-KS) Bi. Hellen Opwapo, amekaririwa akisema kuwa mojawapo ya miradi ya ODM-KS ni kuanzisha elimu ya kisiasa na historia ya Kenya hapa Sweden. Alisema haya wakati ambapo wanachama walikutana ili kupewa ripoti kutoka kwa kamati kuu ya chama hicho. “ODM-KS itatoa elimu ya Siasa na Historia bure kwa Wakenya wote wanaotaka.”
Kwenye maoni yake mwenyekiti, ODM-KS inaamini kwamba wanasasia wanajukumu la kufunganisha ukuzaji wa uchumi na jamii pamoja na kuendeleza maslahi ya wasiojiweza kwanza. Aliendelea na kusema kuwa ODM-KS itaendelea kushirikiana na Wakenya kwenye mipango ya kijamii katika maeneo mbalimbali. Bi. Opwapo aliwahimiza Wakenya kuunga chama cha ODM-K mkono, kwani hicho ndicho chama cha kipekee ambacho kina mpango halisi kwa Wakenya.
Wakati huo huo, Bi. Sofia Njoroge ambaye ni Mweka hazina wa ODM-KS, aliwashukuru Wakenya kwa kutoa fedha na kumsaidia mama mmoja mjane, kule Korogocho mjini Nairobi, ambaye pia ameachiwa watoto wanne yatima. Aliwahimiza Wakenya kuendelea na kuwasaidia wasiojiweza kwenye jamii. Aliendelea kusema kwamba Wakenya wajitoe na kujikaza mhanga, ili tujenge nchi yetu ya Kenya. ODM-KS imejihusisha na maswala nyeti ya kisiasa na kutetea jamii ya Wakenya hapa Skandinavia na hata kwingineko.
Kamati ya ODM-KS iliwahimiza Wakenya waendelee na kujiunga na chama cha ODM-K ili kusaidia kiutoa serikali ya Rais Kibaki, ambayo imekuwa ikiwanyanyasa wananchi wa Kenya. Bi Opwapo alinukuliwa akisema kwamba Tawi lake litaendelea na kuwa na uhusiano na jamii na kusambaza habari za ODM-K hapa Skandinavia. “Tutaendelea kutoa huduma bora kwa Wakenya, na wanakaribishwa kwenye ofisi yetu huko Högbergsgatan 48, na wawe na uhuru wa kupiga simu wakati wowote kwa sababu ODM-K ni chama cha Wakenya.”
Hivi karibuni, ODM-KS itaanza kutoa elimu ya Sayansi ya Siasa na historia ya Kenya. Wakenya wanakaribishwa sana. Bi. Opwapo alisema kwamba elimu ni swala nyeti sana kwa jamii, na ODM-KS itawahudumia watoto, vijana na hata watu wazima. Alisema kuwa jambo hili ni la muhimu sana kwa kuwa mradi huu utakuwa ni wa kuangamiza ujinga kati ya jamii ya Wakenya na hata Waswidi kwa jumla.
Aliwahimiza Wakenya kuungana na kufanya kazi kwa umoja ili kujenge nchi yetu ya Kenya. Katika waraka huo, Bi Opwapo alisema kwamba ni aibu kubwa sana, kuona Ubalozi wa Kenya hapa Skandinavia umekataa kata kata kuwahudumia Wakenya. Alimuhimiza Balozi wa Kenya hapa Scandinavia Bi. Purity Muhindi, kufungua mlango kwa Wakenya kwani alitumwa hapa kuwahudumia. Hivi majuzi, Wakenya wengi wamelalamika wakisema kuwa, hakuna ufahamiano kati ya Ubalozi na Wakenya.
Munala Wa Munala (kajamii@yahoo.com)
Bwana John Githongo: Shujaa au Msaliti?
Kuangamiza ufisadi ilikuwa mojawapo ya ahadi Rais Kibaki aliwapa Wakenya alipochukuwa uongozi wa nchi mwisho wa mwaka 2002. Kuthibitisha kwamba vita dhidi ya ufisadi vingepigwa, alibuni Idara ya Maongozi Bora na Maadili, akamteua Bw. John Gothongo kama Katibu wa Kudumu, mwanzoni mwa 2003.
Bw. Githongo alipewa ruhusa na rais Kibaki kuchunguza na kuripoti kwake moja kwa moja, mambo yote yanayohusu ufisadi nchini. Fichuo kubwa kabisa katika kazi yake lilikuwa ni lile la kashfa ya rushwa ya Anglo-Leasing, iliyogharimu nchi yetu hasara ya mabilioni ya shilingi. Kashfa hii ilihusu miradi ya mazimwi yaliyobuniwa na mawaziri kadhaa na wafanyabiashara humo nchini na ng’ambo. Miradi hii haijatekelezwa hadi leo.
Bw. Githongo alijiuzulu mwanzoni mwa mwaka wa 2005 akidai kwamba rais Kibaki, mawaziri fulani na maofisa wakuu serikalini, hawakumpa sapoti kwa kazi yake ya kufichua rushwa. Alitorokea Uingereza, na mengi yalisemwa baadaye kwamba Githongo angebaki nchini, ili kuelezea ukweli wa kashfa hii na kadhalika. Tangu aingie ukimbizini, Githongo amefichua vitu vingi na kuhojiwa kwenye njia mbalimbali za mawasiliano. Hivi majuzi, serikali ya Kenya ilidai kwamba baadhi ya wale waliotajwa na hata sauti zao kunaswa na Githongo kwenye tepurekoda, hawakufanya makosa. Kwa hivyo, “walisafishwa” ili kutolewa katika lawama ya Anglo Leasing.
Tunaposubiri uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu, tukumbuke ahadi ya Rais Kibaki ya kumaliza kabisa ufisadi, na udhaifu aliyoonyesha hadi sasa. Tumkumbuke pia Bw. Githongo na majukumu aliyopewa hapo mwanzoni, kisha kuwekwa mapresha na maofisa serikalini. Ni hasara na aibu kwa nchi yetu, kwani sasa Bw. Githongo ni mkimbizi nchini Kanada, ingawa angekuwa nyumbani akifanya kazi aliyopewa na rais Kibaki. Watu fulani wanasema kwamba Githongo ni shujaa kwa kufichua kashfa ya Anglo Leasing na mengineyo, bali wengine wanamuona kama mhalifu na msaliti, kwa kuwafichua “ndugu zake”. Kwa watu hawa, rushwa ni hali ya kawaida nchini.
Jared Odero
John Githongo: http://http://en.wikipedia.org/wiki/John_Githongo
Anglo Leasing: http://en.wikipedia.org/wiki/Anglo_Leasing_Scandal
“Wakenya ni Bure” Asema Rais Kibaki
Kwa mara nyingine tena, Rais wa Kenya Bw. Kibaki amewatusi Wakenya kuwa watu bure na watu duni ambao hawahitaji kusamehewa na kuhurumiwa. Kila Mkenya anaelewa wazi msaada adhimu unaofanywa na Bw. Kibaki, kwani utawala ni mzigo usiyobebeka kwa urahisi. Wote twajua kuwa Bw. Kibaki amejaribu kupiga hatua kwa kuimarisha uchumi wa nchi yetu.
Bila shaka, Wakenya hawafurahishwi na tabia ya Rais Kibaki, ambayo ni ya maringo, matusi na kujivunia mambo madogo madogo. Rais wa Kenya ametoa amri kwa sauti kali ya kivita kwa Mkenya yeyote atakayeenda kinyume cha sheria. Kwa maoni yake, amesema wahalifu wote wasihurumiwe hata kidogo. Kama mjuavyo, Wakenya wengi wanaoshikwa na polisi ni masikini na hawana sauti ya pesa. Wengi wao hawafikishwi kotini ili wajitetee.
Wakati alipokuwa akizindua sanamu ya Dedani Kimathi jijini Nairobi, rais aliendelea na tabia yake ya kawaida ya kujidai kwa kulainisha uchumi, na kuongezea matusi yake ambayo Wakenya wameanza kuyazoea. Aidha, aliendelea kuwahimiza Polisi kuwamalizia mbali majambazi wote. Hii ni kusema, ueni wakorofi wote ambao wengi wao ni masikini hohe hahe. Tangu lini Rais wa Kenya alipewa haki ya kutoa amri kama hiyo?
Kama tulivyowaeleza kwenye makala yetu ya juzi kuhusu uchumi, tuliona wazi kuwa uboreshaji wa maisha ya Wakenya sio tu kwa kuimarisha uchumi, bali kuna sekta zingine ambazo zimesahaulika kabisa. Serikali yetu inaendelea kusambaza uvumi kuwa Kenya inaendelea vyema. Ukweli ni kwamba maskini anaendelea kuteseka kila siku.
Hivi majuzi, nilipata fursa ya kwenda Nairobi kuwatembelea watu wa makazi duni kwenye kitongoji cha Korogocho. Amini usiamini, yale nilioyaona yalifungua ukurasa mpya kwa maisha yangu. Wakaaji wengi wa kitongoji hicho wako katika hali mbovu sana, ambayo sitaongelea kwenye makala haya.
Wakenya wengi wanafahamu Polisi na majukumu yao. Wao ni chombo cha serikali chenye nguvu ya kisheria ya kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa, na usalama wa raia na mali zao unakuwepo. Polisi wanapewa mafunzo ya sheria na ukakamavu ili kuwadhibiti raia wakorofi. Miongoni mwa majukumu yao, ni kuwaelimisha raia kuhusu makosa mbalimbali yanayofanyika, kwa sababu sio makosa yote yanapelekwa mahakamani.
Kwa miaka kadhaa sasa, baadhi ya Polisi wanawajibika kinyume cha kiapo cha utii wa sheria ya kuwatumikia Wakenya, yani Utumishi kwa wote. Wengi wao wanashirikiana na wahalifu na kuvunja sheria na kuwadhulumu Wakenya bure.
Mapolisi wengi sana wameingia dini ya Rushwa ambayo inakubali toa kitu kidogo na kuwalazimisha Wakenya kushirikiana nao katika mchezo wao mchafu. Haitoshi, baadhi ya Polisi hutumia lugha za ubabe, vitisho na kutumia nguvu hata wakati hakuna sababu ya kutumia nguvu kutatua kosa.
Matokeo yake ni kama tunavyoona sasa hivi. Raia wamejichukulia sheria mikononi. Baadhi ya Wakenya wasio na hatia, wamekuwa wakipewa adhabu kubwa sana. Wengi wao ni watu hohe ambao hawajiwezi hata kidogo. Polisi wa Kenya hawaelewi haki za kibinadamu na ingekuwa vema kama wangeelimishwa ili kuboresha kazi yao. Isitoshe, matusi mengi wanayotumia ni kama yale ya Bw. Kibaki.
Je! Ni vipi leo tumekuwa wapumbavu na miaka mitano iliyopita tulikuwa malaika? Hali hii ngumu tutavumilia hadi lini?
Munala wa Munala (kajamii@yahoo.com). Habari zaidi kutoka kwa IPPMedia.com (10/02/2007)
Je Kuimarisha Uchumi Itaipa Serikali Ya Kibaki Kura?
Mara kwa mara Rais Kibaki na wafuasi wake wanakaririwa katika njia za mawasiliano wakisema kwamba wamefanya bidii kufufua uchumi nchini Kenya. Kwa sababu hii, wanafikiri ya kwamba wanapaswa kuridishwa serikalini baada ya uchaguzi mkuu, mwishoni mwa mwaka huu.
Ni kweli serikali hii inafanya bidii kuboresha huduma mbalimbali na kuimarisha sekta ya kilimo, inayotegemewa na Wakenya wengi. Serikali pia imefanya juhudi kuyapa majimbo yote ya uchaguzi, mamilioni ya fedha, ili miradi tofauti ianzishwe. Hii ni sawa, isipokuwa kuimarisha uchumi isiwe tu ndio mahubiri ya kutafuta kura kwa wananchi.
Hapa Sweden, matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana yalistaajabisha serikali ya wakati huo (Social Democratic Party) iliyotawala miaka 12, na hata kuimarisha uchumi. Swala ambalo liliwaangusha lilikuwa ni la kuwapa watu kazi, ila hawakulishugulikia, wakidhani kwamba Waswidi walifurahia uchumi uliyo imara. Wapinzani wao nao walizunguka zunguka nchini wakihubiri na kuahidi kazi, kama wangepigiwa kura.
Cha ajabu ni kwamba waaumini wengi wa serikali hiyo ya zamani waliwapa kura zao muungano wa upinzani, ambao sasa unatawala. Wengi walikuwa wameshachoka na maneno ya waziri mkuu wa zamani, kwani alianza kuwa na kiburi. Alikuwa na hakika wangepata kura na kurudi serikalini, kulingana na rekodi yao nzuri ya uchumi.
Tukirudi nchini Kenya, twaona kwamba rais Kibaki anaonyesha mtindo huo huo wa kiburi na maringo. Nampongeza kwa juhudi zake, isipokuwa kuna wakati maneno yake ni yale ya mtu aliyeanza kujisifu kabla hata ya kumaliza mbiyo. Rais huwa anawakemea wapinzani wake kwa kuwaita “Pumbavu, Mavi ya Kuku, Bure Kabisa” na kadhalika. Huu ni ujeuri mkubwa, kwani kiongozi anapaswa kuepuka matusi, hata kama anashutumu. Isitoshe, waziri wa Sheria Bi. Martha Karua, huwa hafichi ujeuri na ukaidi wake, anapowakemea wapinzani wa serikali.
Ukosefu wa kazi nchini Kenya ni hofu kubwa kwa wananchi wengi. Licha ya hayo, kuna ushahidi kwamba watu fulani wanaajiriwa kulingana na makabila yao, mapendeleo au uhusiano wao kisiasa. Hii inazidisha pengo katika mapato ya kibinafsi. Uwongo mkubwa wa serikali ya Kibaki katika kampeni za 2002, ni ahadi ya kubuni kazi kwa watu laki tano kila mwaka. Ingawa vijana wengi wanakamilisha masomo kila mwaka, wengi wao hawapati kazi kamwe.
Mwaka jana waziri wa ujenzi wa barabara Bwana Nyachae, alizipa sehemu zinazo sapoti serikali pesa nyingi za kutunza mabarabara, zaidi ya sehemu za upinzani. Hii ni kinyume cha ahadi ya rais Kibaki kuwatumikia wote bila ubaguzi. Ikiwa bajeti ya miradi ya maendeleo itaendelea kugawanywa kwa hali hii, basi inathibitisha hofu ya wengi kwamba serikali haina haja ya kusawazisha utajiri ili kuangamiza umaskini.
Serikali ya rais Kibaki inapaswa kufikiria na kurekebisha hali mbaya ya usalama inayotisha wananchi kutokana na ongezeko la ujambazi, ili kuwapa amani. Hata kama wito wa rais ni “taifa la kazi”, anakumbushwa kwamba raia wengi wako mbali na hali hii, na watafikiria njaa, umaskini na mateso waliyopitia kwa miaka mitano, watakapo piga kura.
Jared Odero (Tuma maoni kwa: kajamii@yahoo.com)
-
Archives
- January 2009 (2)
- December 2008 (6)
- November 2008 (14)
- October 2008 (3)
- September 2008 (2)
- June 2008 (1)
- May 2008 (1)
- April 2008 (5)
- March 2008 (7)
- February 2008 (11)
- January 2008 (13)
- December 2007 (13)
-
Categories
-
RSS
Entries RSS
Comments RSS